Psalms 38

Maombi Ya Mtu Anayeteseka

(Zaburi Ya Daudi)


1 aEe Bwana, usinikemee katika hasira yako,
wala kuniadhibu katika ghadhabu yako.

2 bKwa kuwa mishale yako imenichoma,
na mkono wako umenishukia.

3 cHakuna afya mwilini mwangu
kwa sababu ya ghadhabu yako,
mifupa yangu haina uzima
kwa sababu ya dhambi zangu.

4 dMaovu yangu yamenifunika
kama mzigo usiochukulika.


5 eMajeraha yangu yameoza na yananuka,
kwa sababu ya upumbavu wa dhambi zangu.

6 fNimeinamishwa chini na kushushwa sana,
mchana kutwa nazunguka nikiomboleza.

7 gViuno vyangu vimejaa maumivu yaunguzayo,
hakuna afya mwilini mwangu.

8 hNimedhoofika na kupondwa kabisa,
nasononeka kwa maumivu makuu ya moyoni.


9 iEe Bwana, yote ninayoyaonea shauku
yako wazi mbele zako,
kutamani kwangu sana
hakufichiki mbele zako.

10 jMoyo wangu unapigapiga,
nguvu zangu zimeniishia;
hata macho yangu yametiwa giza.

11 kRafiki na wenzangu wananikwepa
kwa sababu ya majeraha yangu;
majirani zangu wanakaa mbali nami.

12 lWale wanaotafuta uhai wangu
wanatega mitego yao,
wale ambao wangetaka kunidhuru
huongea juu ya maangamizi yangu;
hufanya shauri la hila mchana kutwa.


13 mMimi ni kama mtu kiziwi, asiyeweza kusikia,
ni kama bubu, asiyeweza kufungua kinywa chake,

14 nimekuwa kama mtu asiyesikia,
ambaye kinywa chake hakiwezi kutoa jibu.

15 nEe Bwana, ninakungojea wewe,
Ee Bwana Mungu wangu, utajibu.

16 oKwa kuwa nilisema, “Usiwaache wafurahie,
wala wasijitukuze juu yangu
mguu wangu unapoteleza.”


17 pKwa maana ninakaribia kuanguka,
na maumivu yangu yananiandama siku zote.

18 qNaungama uovu wangu,
ninataabishwa na dhambi yangu.

19 rWengi ni wale ambao ni adui zangu hodari,
wale wanaonichukia bila sababu ni wengi.

20 sWanaolipa maovu kwa wema wangu
hunisingizia ninapofuata lililo jema.


21 tEe Bwana, usiniache,
usiwe mbali nami, Ee Mungu wangu.

22 uEe Bwana Mwokozi wangu,
uje upesi kunisaidia.
Copyright information for SwhKC